KESI ya mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa
mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten Daud Mwangosi
inayomkabili Pasificus Cleophace Simon imeendelea kusikilizwa leo katika
Mahakama Kuu kanda ya Iringa ambapo mashahidi wawili upande wa Jamhuri waliweza
kutoa ushahidi wakiongozwa na wawendesha mashtaka wa serikali Sunday na
Ladslaus Komanya.
Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Paul
Kihwelo shahidi namba tatu ambaye ni hakimu katika mahakama ya Mwanzo Dodoma
mjini Flora Mhelela ameieleza mahakama kuwa Pasificus alifika ofisini kwake
wakati alipokuwa hakimu katika mahakama ya mwanzo ya Bomani iliyopo Iringa
mjini kwa ajili ya maungamo juu ya kesi inayomkabili.
Ameiambia mahakama kuwa mnamo Septemba
05, 2012 mtuhumiwa kwa kuongozwa na askari ambaye hakumkumbuka jina, alifika
ofisini kwake kwa ajili ya maungamo juu ya kesi inayomkabili ambapo ulikuwa ni
muda wa saa 07:24 mchana.
Amesema baada ya kupata taratibu
zinazotakiwa kufuatwa wakati wa utoaji maelezo mtuhumiwa alikiri kuwa amehiari
mwenyewe kutoa maelezo ambapo baada ya kukaguliwa katika mwili wake alikutwa na
kidonda kibichi kidoleni pamoja na majeraha makavu.
“Mtuhumiwa aliniambia kwamba mnamo
Septemba 2, 2012 ilitokea kazi ambayo alipangiwa kwenda Nyololo ambako kulikuwa
na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walikwenda kufanya
mkutano.
“Aliendelea kusema kuwa kama ilivyo
kawaida kwa ajili ya ulinzi na usalama, kwamba hawakutakiwa kufanya mkutano huo
kwa kuwa haukuwa rasmi. Mkutano ulikuwa unazuiliwa kwa sababu kulikuwa na tukio
la sensa” ameeleza shahidi namba tatu.






.jpg)