Zahanati ya kijiji cha Rungemba |
WAHUDUMU wa afya katika
zahanati ya Rungemba Kata ya Rungemba Wilaya ya Mufindi katika Mkoa wa Iringa
wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi nyakati za usiku kwa sababu
ya kukosa mwanga.
Hayo yamebainishwa na muuguzi
katika zahanati hiyo Suzan Mhongole alipokuwa akiongea na gazeti hili jana juu
ya ugumu wa kazi yao nyakati za usiku.
Mhongole amesema wanalazimika
kutumia kurunzi nyakati za usiku hasa pale anapofika mama mjamzito mwenye
uchungu wa kujifungua au mgonjwa anayehitaji huduma ya haraka.
“Tulikuwa na mwanga unaotokana
na jua (solar power) lakini zimeharibika na hatujui tatizo ni nini kwani hata
wakija mafundi hawatuelezi tatizo ili ufanyike utaratibu wa kutatua tatizo
hilo.
“Kijiji kilileta mafundi lakini
hawakutueleza tatizo ni nini. Tunafanya kazi katika mazingira ya hatari sana
kwani ni hatari hata kwa mama na mtoto pale anapojifungua au mgonjwa ambaye
anahitaji huduma ya haraka” amesema Mhongole.
Ameeleza kuwa shida yao kubwa
katika sehemu yao ya kazi ni mwanga kwani hawawezi kufanya kazi vizuri nay a
kuridhisha kama hawana mwanga na kuiomba serikali kuwafikiria katika hilo.
“Tumewaambia wananchi kuwa
wajitahidi pale wanapopata tatizo wanapokuja kwenye matibabu wafike na taa
lakini wakati mwingine inakuwa ni dharura mno wanasahau kwa hiyo inatulazimu
kuanza kutafuta betri za kurunzi usiku huku mgonjwa akikosa huduma hadi pale
zinapopatikana betri. Mazingira kwa ujumla mi magumu” alisema.
Hata hivyo utafiti uliofanyika
na gazeti hili katika kijiji hicho umebaini kuwapo kwa uhaba wa mafuta ya taa
ambapo ni chanzo cha wagonjwa kutofika na taa kwenye zahanati pale wanapohitaji
huduma nyakati za usiku.
No comments:
Post a Comment