KLERUU

KLERUU
KLERUU

Ibada

Ibada

Sunday, December 14, 2014

Uchaguzi Serikali za Mitaa waingia dosari Ngome



UCHAGUZI wa serikali za Mitaa katika Mtaa wa Ngome Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa umeanza kwa dosari licha ya kulazimika kuanza saa 6:04 mchana kutokana na kucheleweshwa vifaa vya kupigia kura.

Licha ya vifaa vya kupigia kura kuchelewa, bado ilitokea dosari katika karatasi za kupigia kura kwa kile kilochoonekana kwa baadhi ya majina ya waliogombea ujumbe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoonekana kwenye karatasi za kupigia kura na badala yake yakaingizwa majina ya watu wengine ambao hawakujaza fomu za kugombea.

Sambamba na hilo kwa upande wa wagombea kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa na kosa la waliogomea viti maalum kuingizwa jina la mwanaume aliyegombea ujumbe huku mwanamke aliyegombea viti maalumu uingizwa kwenye karatasi la wagombea wa ujumbe.

Sababu hizi zimemlazimu wakala wa Chadema kutokubaliana na utaratibu huo na kutaka utolewe ufafanuzi zaidi kabla ya kuanza zoezi la upigaji kura na kumlazimu msimamizi wa uchaguzi wa kituo hicho kumpigia simu ofisa mtendaji wa Kata ili aweze kutolea ufafanuazi  jambo ambalo pia lilimlazimu ofisa mtendaji kurudisha karatasi kwa mkurugenzi ili zifanyiwe marekebisho.

Baada ya maelezo ya ofisa mtendaji wa Kata ya Kihesa Wilbert Chahe kuwa kuna makosa katika karatasi hizo, wananchi walipandisha hasira na kumzingira ofisa huyo jambo lililowawalazimu vijana wa Chadema kumnusuru ili aweze kurudisha karatasi zikarekebishwe.

“Ndugu zangu wananchi na wapiga kura, nawaombeni kuwe na uvumilivu kuna tatizo tumeligundua kwenye karatasi hizi lakini sisi ni watendaji tu, inabidi nirudishe kwa Mkurugenzi ili yafanyike marekebisho. Kwa nawaombeni muwe wavumilivu ili nishughulikie suala hili” amesema Chahe.

Baada ya maelezo hayo wapiga kura walianza kupiga kelele huku wakimzingira, “acheni uzuhi mmeanza mizengwe ili kukwamisha uchaguzi, huo ni mpango wa makusudi mlioupanga ili uchaguzi usifanyike, tumechoka kuburutwa” zimesikika sauti hizo huku wengine wakisema “umetumwa wewe, kawaambie waliokutuma kwamba tunajitambua” zimesikika sauti hizo.

Wakati wapiga kuwa wakisubiri karatasi kwa ajili ya kupiga kura, vijana walioaminika kuwa ni viongozi wa chama cha Mapinduzi (CCM) walifika katika eneo la kituo cha kupigia kura katika Mtaa huo na kuanza kuanza ushawishi kwa wapiga kura kuipigia CCM jambo lililowatia hasira baadhi ya wapiga kura na kutoa taarifa polisi.

Askari polisi aliyekuwa akilinda usalama katika kituo hicho aliwatuma baadhi ya vijana ili waaondoe viongozi hao mahala hapo kiustaarabu lakini viongozi hao walianza kutumia nguvu kuwa hakuna wakuwatoa nakutangaza kupigana kufa na kupona.

Mmoja aliyekuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeusi anayeaminika kuwa ni katikabu wa Umoj wa vijana Chama cha Mapinduzi (UV-CCM) Wilaya ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Kilimani alianza kutaka kurusha ngumi jambo lililomlazimu askari wa ulinzi kuomba msaa kwa maaskari wenzake.

Wakati mawasiliano ya askari na maaskari wengine yanaendelea, vijana wa Chadema ambao wanaaminika kuwa ni walinzi (red-brigade) walituliza upepo ulioanza kuchafuka na kuwataka watu kuwapuuza viongozi hao kwa kuwa nia yao si nzuri katika uchaguzi.

Kila mara red brigade walionekana kuwatuliza vijana waliokuwa na hasira kutaka kutwangana na viongozi wa CCM ili kuwawezesha wapiga kura kuwa na amani.

Hadi polisi wanafika katika eneo la tukio, walikuta vijana wa Chadema wameshayaweka mazingira katika hali ya usalama na kuwaeleza polisi kuwa viongozi hao walikimbia baada ya kuona gari la polisi linakuja na polisi wakawataka kutoa taarifa haraka pale watakapoonekana katika mazingira hayo tena.

Wakati huo huo wananchi wakisubiri karatasi za kupigia kura, baadhi ya wapiga kura waliokuwa wamekaa chini ya mti walisikika wakisema kuwa usiku wa kuamkia jumapili kuna baadhi ya watu wanaoaminika kuwa ni wanachama wa CCM walikuwa wanapita wakigawa shiligi elfu tano na maharage kilo moja moja kwa wapiga kura ili kuwashawishi wapiga kura kuipigia kura za ndiyo.

Hata hivyo wananchi wametaka kujua mwisho wa kupiga kura kutoka na kuchelewa kuanza lakini msimamizi wa kituo amesema atawasiliaa na viongozi wa juu ili waone kama wanaweza kuongeza muda wa kupiga kura katika kituo hicho.

No comments:

Post a Comment