BAADHI ya waajiri wanalalamikiwa
kuwanyanyasa wafanyakazi wao pindi wanapojiunga na vyama vya wafanyakazi ili
kuwakatisha moyo wa kutafuta haki zao.
Haya yamezungumzwa na Mohamed Sadick
alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Kanda wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi,
Nishati, Ujenzi na Kazi zingine (TAMICO) uliofanyika katika ukumbi wa
jengo la shirikisho la vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Iringa.
Sadick amesema kazi ya vyama vya
wafanyakazi si ndogo kwa kuwa hufanya kazi zaidi ya vyama vya siasa kwa kudai
haki ya kweli kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta mbalimbali bila kujali
idikadi na bila ubaguzi wowote.
Amesema pamoja na kuwa wafanyakazi wana
haki mbalimbali kazini, wapo baadhi ya waajiri ambao huwatishia wafanyakazi wao
pale wanapojiunga na vyama vya wafanyakazi wakitaka kuwakatisha tamaa ya kudai
haki zao ili waendelee kunyonywa.
Amewataka viongozi wa vyama vya
wafanyakazi kuwa na msimamo wa dhati na kutokubali kubadilika kutokana na
magumu wanayokutana nayo wawapo katika harakati za kudai na kusimamia haki za
wafanyakazi wao.
“Viongozi wa vyama vya wafanyakazi
msifanye kazi kwa kutaka kusifiwa. Fanyeni kazi kwa kujituma kwa kutafuta haki
za wafanyakazi.
“Kiongozi lazima astahimili kwa sifa
zote ama kwa kusifiwa ama kutosifiwa na pia astahimili hali zote anazokutana
nazo kwa waajiri pale anapokuwa akiwajibika kikazi kwa ajili ya haki za
wafanyakazi” amesema Sadick.
Mzee Sadick ambaye aliwahi kuwa katibu
wa chama hicho cha wafanyakazi ambaye pia ni mstaafu amesema kiongozi
anayependa rushwa kutoka kwa mwajiri, anawaangamiza wafanyakazi waliompa
dhamana ya kuwa msemaji wao na kwamba kiongozi wa namna hiyo hafai.
Akisoma taarifa ya chama hicho kwa niaba
ya Katibu wa chama hicho Juma Bwikitila amesema moja ya changamoto kwa vyama
vya wafanyakazi ni kuongozwa na viongozi wasio na uwezo.
Bwikitila amesema kuwa viongozi wakikosa
uwezo baadhi ya waajiri wanatumia udhaifu huo kuwafukuza wafanyakazi wao
wanapojiunga na vyama vya wafanyakazi.
Mkutano huo ulikwenda sambamba na
uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa chama hicho ambapo Denis Daniel Malawa kutoka
sekta ya barabara Mkoa wa Iringa amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Wilaya huku
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Kanda wakiwa Mercy Chindongo kutoka sekta ya ujenzi,
Joyce Lyatuu – kazi nyingine wakati sekta ya migodi na nishati zikiachwa wazi
hadi hapo watakapopata wawakilishi kutokana na kukosa wajumbe kwenye mkutano
huo.
Kamati ya utendaji Wilaya viongozi
waliochaguliwa ni Daniel Panjinga Msalilwa (ujenzi), Shabani Omary Mtunguja
(shirika la nyumba), Sheila Mwinyimkuu Mwinyiheri (sekta ya barabara Njombe),
Subira Anyesile Maikema huku sekta za migodi na nishati zikiachwa wazi.
Kamati ya wanawake viongozia
waliochaguliwa ni Rose Wales Makoti kutoka Songea akichaguliwa kuwa Mwenyekiti
na Felista Adelgori Banda kutoka sekta ya barabara Mkoa wa Iringa akichaguliwa
kuwa Katibu.
Waliochaguliwa kuwa wajumbe wa kamati ya
wanawake ni Julieth James na Dynes Panjinga Msalilwa huku Ibrahimu Mianzi,
Elida Joseph Ngunguru na Mukakalo Charles Mukakalo wakichaguliwa kuwa kamati ya
vijana.
Wajumbe wa wanne wa Mkutano Mkuu
waliochaguliwa ni Edesius Silvanus Kangole, Omary Said Chitawala, Mercy Stanlay
Chindongo na jila na nne linasubiriwa kupatikana kutoka sekta ya migoti.
TAMICO ni miongoni mwa shirikisho la
vyama vya wafanyakazi Tanzania chini ya mwavuli wa TUCTA.
No comments:
Post a Comment