VIJANA Wakristo Wakatoliki wametakiwa
kutokujiingiza katika vitendo vya ufisadi na badala yake wametakiwa kutumia
uhuru waliopewa na Mungu ipasavyo bila kuwakwaza wengine na kwamba viongozi
wanaoshindwa kutekeleza majukumu katika haki ni wasaliti wasiowatakia mema
wengine.
Haya yamezungumzwa na Jaji Mstaafu
Raymond Mwaikasu alipokuwa akiwahutubia vijana wakati wa sherehe za mzimamizi
wao Mt. Yohane Bosco zilizofanyika katika ukumbi wa Don Bosco Parokia ya Mkwawa
Jimbo lringa.
Jaji Mwaikasu amesema ufisadi umekuwa ni
tatizo kubwa katika serikali ya Tanzania na kwamba unasababishwa na watu wasiyo
na huruma, wabinafsi, wasiomuogopa Mungu kuwa waroho kupindukia.
Amewataka vijana kutotumia utashi wao
vibaya pamoja na kutotumia uhuru wao kutenda maovu.
“Tambueni kwamba hapa duniani kuna mvuto
wa aina mbili, mvuto wa shetani na mvuto wa Mungu. Msifuate mkumbo. Utashi wenu
mkiutumia vibaya utawaingiza pabaya” amesema jaji Mwaikasu.
Amesema licha ya kuwa binadamu
anatofautiana na wanayama wengine, tofauti hiyo itimike katika kutenda mema na
kupiga vita ukatili, ubaguzi, chuki, unyanyasaji na dhuruma.
Pia amesema binadamu anadaiwa kutenda
matendo mema kwa wengine na kuwa chachu ya amani, umoja na mshikamano ili
kuwezesha wengine kuishi katika furaha.
Amesema kukosa maadili ni kusababisha
vitendo vichafu kama wizi, ujambazi na kujiingiza katika vikundi viovu kama “panya
road” na kwamba mafundisho ya Mungu ni chachu ya mahusiano mema na wengine.
“Pigeni vita wizi wa mali ya umma,
dhuruma, ubadhilifu, vitendo vya utoaji mimba, ujambazi, udanganyifu, hila,
udini na ukabila, rushwa, ukatili na uonezi wa haki.
“Jengeni mahusiano mazuri ili tuweze
kutoa haki pale penye unyanyasaji. Jiungeni na wenye taaluma ili muwe watendaji
wazuri. Zingatieni umuhimu wa maisha yenu ya kiroho” amesema.
Kumbukumbu ya msimamizi wa vijana Mt.
Yohane Bosco hufanyika Januari 31 ya kila mwaka.
No comments:
Post a Comment