KLERUU

KLERUU
KLERUU

Ibada

Ibada

Saturday, June 20, 2015

CCM ni jinamizi linalotakiwa kuondolewa: Mbunge

Mbunge wa viti maalum wa jimbo la Mjini Magharibi – Zanzibar Maryam Salum Msabaha aliyejitanda nguo kichwani akisikiliza kwa umakini namna watoto wanavyolelewa. Mwenye kofia ni Sista Cecilia kitasile mlezi wa watoto hao.




BARAZA la wanawake wa Chama cha Demkrasia na Maendeleo (Bawacha) Mkoa wa Iringa wametoa msaada wa vitu mbalimbali katika kituo cha watoto yati cha Mersino Meraddin Migoli pamoja na fedha tasilimu kiasi cha shilingi 1,645,000/=.

Msaada huo umetolewa wakati walipotembelea kituoni hapo kama ni sehemu ya kufanya kumbukumbu ya mtoto wa Afrika.

Wakikabidhi msaada huo, Mbunge wa viti maalum wa jimbo la Mjini Magharibi – Zanzibar Maryam Salum Msabaha alibubujikwa na machozi baada ya kuwaona watoto hao na kutoa msaada wa shilingi milioni moja huku Mbunge wa viti maalum Naomi Kaihula akitoa kiasi cha shlingi 550,000/=.

Akizungumza kituoni hapo Maryam Msabaha alisema jamii ina jukumu la kuishi na watoto wasio na wazazi kama familia ili kuwajenge uwezo wa kutengeneza maisha yao kimalezi.

Alisema suala la kulea watoto si la wamisionari pekee bali ni jukumu la kila mtu aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu na kwamba watoto wasibaguliwe.


“Ninatoa kwa nia njema na kwa moyo safi kwani nikiwaona watoto nafarijika mno. Hawa ni watoto wetu sote tunapaswa kuwajibika” alisema Maryam huku akibubujikwa machozi.

Naye Naomi Kaihula alisema Bawacha siyo maneno tu bali ni kufanya kwa vitendo na kwamba mwanamke asiyependa watoto hawezi kuwa na roho nzuri kwa wengine.

“Bawacha siyo maneno tu ila ni kuibeba jamii. Watoto ndiyo amani yetu. Tuwapende kwa moyo na kwa ukarimu wetu” alisema Kaihula.

Akipokea msaada huo, Mlezi wa Kituo hicho Sista Cecilia Kitasile alitoa hisia zake na kusema kuwa ni watu wachache wanaokumbuka watoto na kwamba Bawacha wawe mfano wa kuigwa na wengine.

Kituo hicho chenye jumla ya watoto 76 kinakabiliwa na changamoto ya ukame kutokana na kuwapo kwa shida ya maji kwa muda mrefu jambo linalowapa shida katika malezi na makuzi ya watoto hao.

“Tunashukuru sana kwa ukarimu wenu na majitoleo yenu. Mungu awazidishie pale mlipopunguza na awape nguvu na afya njema kwa ajili ya kutoa huduma kwa wahitaji wengine.

“Tunatatizo kubwa la maji ambalo hatujui ufumbuzi wake. Kama mnavyoona ukame kupata maji kwetu ni shida sana. Pia tatizo lingine ni mwanga. Si kwamba umeme hatuna! Umeme tunao lakini tatizo tunakosa fedha za kulipa bili kwa kuwa hatuna biasha ya kufanya zaidi ya kulea hawa watoto. Tunatumia mwanga wa jua lakini hautoshi na tumekuwa tukikosa mwanga kutokana na mashine kuharibika mara kwa mara” alisema kwa uchungu.

Alieleza kuwa watu wamekuwa hawana utamaduni wa kuwatembelea watoto katika kituo hicho jambo ambalo linawafanya watoto kujiona kama wametengwa na jamii.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara mara baada ya kukitembelea kituo hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha Taifa Kunti Yusuph aliwataka wananchi wa Isimani kutoukumbatia mti wenye miba ili kuepuka majeraha.

Alisema Chama cha Mapinduzi ni mti wenye miita ambao kwa muda mrefu miiba imekuwa ikiwajeruhi Watanzania jambo linalowasababishia maumivu katika maisha yao na kwamba mwaka huu uwe ni mwaka wa kufanya mabadiliko kuachana na miiba hiyo.

“Tupo safarini kutafuta ukombozi kwa mara ya pili dhidi ya udharirishaji unaoendelezwa na CCM kwa zaidi ya miaka 50. Nyerere hakutaka kutengeneza viremba, fulana na kofia kwa kuwa aliona shida ya watanzania si kuangalia sura za viongozi katika vitenge na kofia bali aliona shida ya watanzania ni afya, elimu, ardhi na maisha bora.

“Watanzania tumegawanywa katika makundi mawili ya walio nacho na wasio nacho. Huu ni ubaguzi ndugu zangu. Tusikubali tena kuingia katika matatizo haya na mwaka huu semeni mateso basi. Fanyeni babadiliko, msitishike na vitisho vyao wala msidanganyike tena” alisema Kunti.

Katika hatua nyingine akiwahutubia umati wa watu katika mkutano huo Mbunge wa viti maalum Maryam Msabaha aliwataka wananchi kuikataa CCM kwa moyo wao wote bila kuogopa na kwamba wasidanganyike kwa kila namna.

“Majinamizi ya CCM watakuja kwa njia mbalimbali. Akina mama kueni macho, kataeni CCM kama ukoma. CCM ilikuwa ya baba wa taifa lakini kwa sasa haipo tena. Viongozi waliopo ni walafi tu” alisema.

Kwa upande wake Mbunge wa viti maalum Naomi Kaihula alisema maisha ya watanzania yanazidi kudumaa kutokana na kukosa viongozi katika taifa.

“CCM wameturudisha kwenye ujima. CCM wanapenda sana kuzungumza maneno badala ya vitendo. Mika ya nyuma Isimani kulikuwa na maendeleo ya kilimo lakini hawa jamaa wametuletea jangwa” alisema Kaihula.

No comments:

Post a Comment