JAMII inapaswa kutambua na kujitoa
katika kuwahudumia wanaoishi na VVU na kuwajali kwa kila namna ili waweze
kuishi muda mrefu wakihudumia familia zao.
Haya yamezungumzwa leo na Mkurugenzi wa Chuo
Kikuu Huria kituo cha Iringa Mch. Dkt. Lechion Peter Kimilike alipokuwa
akikabidhi msaada wa vyakula kwa ajili ya kuwasaidia wanaoishi na VVU katika
kituo cha Allamano kilichopo katika Manispaa ya Iringa.
Amesema kazi ya kuwahudumia waishio na
VVU ni ya jamii nzima kwani hali hii inaweza kumtokea mtu yoyote na kwamba
jamii isiwabague, kuwatenga au kuwafanyia vitendo vya kikatili wanaoishi na
maambukizi bali iwafariji na kuwajali kwa kila jambo ili wasikate tama ya
kuishi.
“Kazi hii ni yetu sote. Jamii inapaswa
kutambua kuwa kuwafanyia vitendo vya ukatili watu kama hao ni dhambi na ni kosa
kisheria.
“Ni dhamna potofu kuwafanyia vitendo vya
ukatili watu kama hawa. Jamii iwe na uelewa wa kutosha” amesema Kimilike.
Dkt. Kimilike pia ameitaka jamii
kutambua kuwa kuzaa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi si dhambi bali ni kiumbe kama
walivyo wengine ambaye anapaswa kuishi na kupata mahitaji kama wapatayo
wengine.
“Kuua albino ni wazo potofu na ni baya sana.
Imani hii haikubaliwi wala haiwezi kuungwa mkono na mtu yeyote. Kuwaua watu
kama hawa ni kutenda dhambi tu kwani hawa ni watu kama tulivyo wengine ambao
wanapaswa kupewa haki zote” amesema.
Pia ameiasa jamii kutoa ushirikiano wa
dhati katika kukemia vitendo vya ukatili na kuwafichua wale wote wanaojihusisha
na vitendo hivyo ili waweze kuwajibishwa kisheria.
Akipokea msaada huo kituoni hapo, Mrabu
wa kituo hicho Christopher Kunzugala amesema elimu kwa jamii bado inahitajika
katika kuwahudumia na kuishi na watu wanaoishi na VVU.
Kunzugala amesema kituo kinakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo ya ukosefu wa fedha za kukiendesha na hivyo kuiomba
jamii kwa wale wanaoguswa kujitoa kwa ajili ya kusaidia kazi ya huduma kwa wale
ambao wananishi na VVU.
Amebainisha changamoto
nyingine ni wateja wenyewe kutozingatia kwa dhati maelekezo ya wataalamu na
kusababisha maambukizi mapya jambo linalosababisha utoaji huduma kuwa mgumu.
“Wateja wengi tunaowahudumia ni akina
mama. Akina baba hawajitokezi kwa wingi kupima au kupata ushauri.
“Nafikiri elimu bado inahitajika
kuielimisha jamii ili watu waweze kujitokeza kupima na kupata huduma kuliko
kuogopa na kuishi kwa hofu” amesema Kunzugala.
Club ya HIV/AIDS ya Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania kituo cha Iringa walitoa msaada wa mafuta ya kula, sukari, chumvi na
unga wa sembe ikiwa ni mwendelezo wa msaada waliotoa juzi katika kituo cha
Huduma ya Mtoto kilichopo Ilula Wilaya ya Kilolo katika Mkoa wa Iringa wenye
thamni ya zaidi ya shilingi 1,000,000/=.
No comments:
Post a Comment