UPATIKANAJI wa damu katika hospitali ya
rufaa ya Iringa pamoja na hospitali za wilaya ni tete kutokana na benki ya damu
kuishiwa damu.
Haya yamezungumzwa na mteknolojia wa
maabara Mkoa wa Iringa Mlike Mwalongo alipotakuwa akihojiwa na waandishi wa
habari ofisini kwake leo juu ya upatikanaji wa damu.
Mwalongo amesema hali ya upatikanaji wa
damu ni tete na kwamba hospitali ya rufaa Iringa pekee inahitaji wastaniwa wa unit 210 kwa mwezi ambapo ni sawa na lita 105
kwa mwezi.
Amesema uhaba wa damu unatokana na
kukosa vitenganishi (vitendea kazi) ambavyo vingewasaidia wataalam wa damu
kufika maeno mbalimbali kwa ajili ya kuwaomba wananchi kuchangia.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni hali ya
uchumi ambapo awali walikuwa wakitegemea wafadhili katika ukusanyaji wa damu
kwa wanaochangia lakini kwa wakati huu wamekosa ufadhili na kusababisha damu
kutopatikana kiurahisi.
“Hali ya upatikanaji wa damu kwa wakati
huu ni tete. Damu haitolewi sehemu moja ila watu wanatembea sehemu mbalimbali
kwa ajili ya kwenda kuomba na kutoa damu kwa watu mbalimbali wanaoguswa na
kuchangia.
“Pia tuna uhaba wa dawa za kupimia damu.
Kwa kuwa upatikanaji wa damu ni tete, tunatumia mbadala kupata damu ili
kumuokoa mgonjwa kwa kuwaomba ndugu wa mgonjwa achangie mgonjwa wake vinginevyo
hatuna jinsi” amesema Mwalongo.
Anabainisha kuwa tatizo la damu
linaloikumba hospitali ya rufaa Iringa ni tatizo la kanda nzima ya nyanda za
juu kusini inayojumuisha mikoa sita ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Katavi na
Rukwa.
Kwa mujibu wa Mwalongo hospitali ya
rufaa Iringa hutumia unit 6 hadi 7 kwa siku ambapo ni sawa na kutumia lita 3.5
kwa siku.
Naye ofisa viwango vya maabara Mkoa wa
Iringa Emmy Mkupasi amesema elimu bado inahitajika kwa jamii juu ya uchangiaji
damu kwani kumekuwa na mpishano wa uelewa juu ya kuwapo na benki ya damu.
“Kumekuwa na lugha gongana tangu
walipotangaza kuanzishwa benki ya damu kitaifa. Watu wanadhani kuwa serikali
inatengeneza damu na hivyo kufikiri kuwa damu itakuwepo tu kumbe wasijue kuwa
damu yenyewe ni ya wananchi wenyewe ambao wanaombwa kuchangia.
“Cha msingi tuwaombe wananchi wahamasike
kuchangia damu kwani hatuwezi kujua ni nani atatumia kwa sababu anaweza akaja
ndugu yako au mtoto au yeyote yule wa karibu akaja kutumia. Inapokosekana damu
tutaanza kulaumiana kuwa damu haipo na sisi hatuna namna yeyote kwamba
tungetengeneza damu. Damu ni yenu na ni yetu sote, tuchangie kwa moyo mweupe”
amesema Mkupasi.
Ameeleza kuwa imebainika kuwa
wanaochangia damu kwa kiasi kikubwa kwa Iringa ni wanafunzi wa shule na wa vyuo
na kwamba pale inapotokea shule na vyuo vimefungwa uchangiaji wa damu unapungua
kwa asilimia kubwa.
Hata hivyo amewataka wananchi kuondoa
dhana ya uchangiaji wa damu kuwa ni watu fulani kwani kila mtu anaguswa na pale
anapofika kwa ajili ya kuchangia hupewa elimu kabla ya kutolewa damu.
“Kwa upande wa uchangiaji wa damu
haubagui mtu, awe ni kiongozi wa dini au mwanasiasa wote suala hili linatugusa.
Tuhamasike na kuhamasishana ili tuweze kupata damu ya kutosha.
“Lakini pia elimu bado inahitajika juu
ya uchangiaji wa damu kwani bado haijawafikia wananchi kiwango cha kutosha.
Wanaoelewa sana ni wanafunzi kwa sababu ndio wanaojitokeza mara kwa mara
kuchangia. Tungependa wananchi wote wahamasike ifike siku moja tukasema sasa
inatosha kwa sababu watu wanakuwa wamejitokeza kwa wingi" amesema.
Mkupasi pia amewataka wanahabari kuwa
mfano wa kuigwa na jamii kujitokeza kuchangia damu ili wananchi wapate hamasa
zaidi kwani hali ilivyo sasa ni tete kupita kiasi.
Kutokana na changamoto ya kukosa damu,
wahudumu wa afya wamekuwa wakishutumiwa bila sababu kuwa wanazuia damu jambo
ambalo limekuwa halina ukweli wa kutosha.
Iliwawia vigumu madaktari nahudumu wa
afya katika hospitali ya Wilaya ya Mufindi iliyopo Mafinga pamoja na hospitali
ya rufaa Iringa wakati ilipotokea ajali iliyoua watu 50 katika maeneo ya
Changarawe kule Mafinga wiki lililopita kwa majeruhi waliotakiwa kuongezwa damu
kwani hakukuwa na damu kulinganisha na mahitaji ya watu.
Watu mbalimbali pia wamekuwa na mtizamo
wao kuwa tatizo kubwa la ukosefu wa damu katika hospitali ni ukosefu wa elimu
endelevu kwa umma.
Njowole Musa mkazi wa Iringa mjini
ameliambia mtandao huu kuwa wananchi hawana elimu juu ya uchangiaji wa damu na
kwamba ingekuwa ni elimu endelevu ili wananchi waelewe kuwa jukumu la
upatikanaji wa damu katika hospitali mbalimbali ni la wananchi wenyewe.
“Mimi mwenyewe sielewi lolote juu ya
uchangiaji wa damu lakini wataalamu wetu wangekuwa na utaratibu wa kutoa elimu
kwetu wananchi na ikawa elimu endelevu, sidhani kama leo hii tungezungumzia
suala la uhaba wa damu.
“Au serikali ingeangalia utaratibu wa
utoaji elimu kwa umma juu ya jambo hili tungekuwa mbali mno. Kama pesa ya
kupita kwa wananchi kutolea elimu haipo, serikali ifanye utaratibu wa wale
mafisadi wanaotuibia kodi zetu warudishe tufanyie masuala ya msingi na ya
muhimu kama haya. Tatizo ni elimu tu” amesema.
No comments:
Post a Comment