KESI ya mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa
mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten Daud Mwangosi
inayomkabili Pasificus Cleophace Simon imeendelea kusikilizwa leo katika
Mahakama Kuu kanda ya Iringa ambapo mashahidi wawili upande wa Jamhuri waliweza
kutoa ushahidi wakiongozwa na wawendesha mashtaka wa serikali Sunday na
Ladslaus Komanya.
Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Paul
Kihwelo shahidi namba tatu ambaye ni hakimu katika mahakama ya Mwanzo Dodoma
mjini Flora Mhelela ameieleza mahakama kuwa Pasificus alifika ofisini kwake
wakati alipokuwa hakimu katika mahakama ya mwanzo ya Bomani iliyopo Iringa
mjini kwa ajili ya maungamo juu ya kesi inayomkabili.
Ameiambia mahakama kuwa mnamo Septemba
05, 2012 mtuhumiwa kwa kuongozwa na askari ambaye hakumkumbuka jina, alifika
ofisini kwake kwa ajili ya maungamo juu ya kesi inayomkabili ambapo ulikuwa ni
muda wa saa 07:24 mchana.
Amesema baada ya kupata taratibu
zinazotakiwa kufuatwa wakati wa utoaji maelezo mtuhumiwa alikiri kuwa amehiari
mwenyewe kutoa maelezo ambapo baada ya kukaguliwa katika mwili wake alikutwa na
kidonda kibichi kidoleni pamoja na majeraha makavu.
“Mtuhumiwa aliniambia kwamba mnamo
Septemba 2, 2012 ilitokea kazi ambayo alipangiwa kwenda Nyololo ambako kulikuwa
na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walikwenda kufanya
mkutano.
“Aliendelea kusema kuwa kama ilivyo
kawaida kwa ajili ya ulinzi na usalama, kwamba hawakutakiwa kufanya mkutano huo
kwa kuwa haukuwa rasmi. Mkutano ulikuwa unazuiliwa kwa sababu kulikuwa na tukio
la sensa” ameeleza shahidi namba tatu.
Amesema kuwa, kwa mjibu wa maelezo ya
mtuhumiwa baada ya kufika katika eneo la tukio walikuta watu wengi wafuasi wa
Chadema wamekusanyika ambapo walitoa ilani mara tatu kuwa hawaruhusiwi kufanya
mkutano na watu hawakutawanyika.
Amesema baada ya kuona watu
hawatawanyiki ilitolewa amri kuwakamata viongozi wa Chadema ambapo pia
waliamrishwa kufyatua mabomu ya moshi ili watu waweze kusambaratika.
“Akasema, wakati wa kutumia mabomu,
ndipo aliposikia sauti ya askari ambaye hakumfahamu jina lake akiomba msaada
ndipo aliposikia mshindo mkubwa lakini hakujua unatoka wapi lakini akashtuka
kuwa huenda ni yeye amelipua bila kujua.
“Alisema baadaye walifolenishwa wakagundua
kuwa silaha aliyokuwa amebeba yeye ilikuwa “wrong ranger” bomu halikuwemo ndipo
wakagundua kuwa ndilo lililomuua mwandishi wa habari Daud Mwangosi japo kuwa
yeye alisema hakukusudia” amesema shahidi huyo.
Kwa upande wake shahidi namba nne mwenye
namba G 3212 Lewis Obadia Teikya ambaye ni dereva wa kikosi cha oparesheni
katika jeshi la Polisi, amesema kuwa wakati tukio la kuuawa kwa Daud Mwangosi
yeye alikuwa mtunza ghala la silaha.
Ametoa maelezo mahakamani hapo mbele ya
Jaji Kihwelo Teikya alisema mnamo Septemba 2, 2012 alipigiwa simu na mkuu wa
kikosi cha kutuliza ghasia saa 12:30 asubuhi kuwa awahi katika ghala la silaha
kwa kuwa imetokea dharula katika Wilaya ya Mufindi kijiji cha Nyololo ili
akawakabidhi sialaha askari.
Amesema mingoni mwa askari waliokwenda
kuchukua silaha asubuhi ya tarehe hiyo ni pamoja na Pasificus Cleophace Simon
ambaye anatuhumiwa kwa mauaji ya Mwangosi na kwamba silaha aliyochukua ni namba
040824 ya mlipuko mkubwa ambayo alichukua saa moja asubuhi ya tarehe 02 na
kuirudisha Septemba 3, 2012 saa 9:15 usiku.
“Wakati natoa silaha nilitoa mabomu ya
mshindo mkubwa 15, mabomu ya moshi wa kuwasha 22, risasi sa SMG 60, risasi za
CSS 8 na mabomu ya kutupwa kwa mkono sikumbuki idadi yake.
“Mabomu yote ambayo niliwapatia
hayakurudi ambapo kwa maana nyingine yalitumika wala hakuna hata askari mmoja
aliyerudisha bomu lolote” alisema shahidi namba nne.
Shahidi huyo ameendelea kusema kuwa
wakati matukio hayo yakifanyika kulikuwepo na viongozi wao wa juu ambapo
Kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa wa wakati huo Michael Kamuhanda alikuwemo.
Hata hivyo, amekiri mbele ya mahakama
kwa vitendo kuieleza mahaka kwa kutumia silaha hiyo iliyofikishwa mahakamani
hapo kwa ajili ya ushahidi kuwa silaha hiyo isingeweza kujifyatua kwa kuwa
ufyatukaji wake ni wa hatua (process).
Kutokana na shahidi namba tano ambaye
kuwa na hudhuru ya kuuguliwa waaendesha mashtaka waliiomba mahakama shauri hilo
liahirishwe hadi pale litakapopangiwa tarehe nyingine katika kikao
kitakachofuata na kwamba kielelezo namba 5 na namba 5 vikabidhiwe kwa jeshi la
polisi kwa ajili ya kutunzwa hadi pale vitakapohitajika tena kwa ajili ya
ushahidi.
Jaji ameahirisha shauri hilo hadi pale
litakapopangiwa tarehe na msajili wa mahakama katika kikao kijacho na mtuhumiwa
amerudishwa rumande.
No comments:
Post a Comment