Polisi nchini Tanzania wanawazuilia
watu watatu wanaotuhumiwa kuhusika shambulio katika msikiti mmoja mjini
Mwanza magharibi mwa nchi hiyo.
Watu watatu, akiwemo Imam,
walifariki wakati wa shambulio hilo lililotekelezwa katika msikiti wa
Rahman wakati wa swala ya usiku siku ya Jumatano.
Kwa mujibu wa
kamanda wa polisi jijini humo, Ahmed Msangi, uchunguzi wa mwanzo
umebaini kwamba mauaji hayo yalifanywa kwa kutumia mapanga na kuongeza
kuwa, polisi wanachunguza chanzo cha shambulizi hilo.
Baadhi ya walioshuhudia tukio hilo, wamesema shambulio hilo lilitekelezwa na kundi la watu wasiopungua 15.
Hakuna aliyedai kuhusika katika shambulio hilo.
Tukio
jingine la mauaji ya kutumia silaha pia limetokea katika mkoa wa Pwani
wilaya ya Mkuranga ambapo askari polisi aliyefahamika kwa jina la
Sajenti Kinyogoli ameuawa na watu wasiojulikana.
Matukio hayo yote
yametokea wiki hii kulipoibuka taarifa kwenye mtandao wa Twitter juu ya
kikundi kilichojitambulisha kama wafuasi wa mtandao wa kigaidi wa
Islamic State wakifanya mazoezi eneo la Tanga, kaskazini mashariki mwa
Tanzania.
Chanzo: bbc swahili
No comments:
Post a Comment