Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje Mch. Peter Msigwa akiongea na waandishi wa habari juu ya fedha za MCC. |
SIKU chache baada ya Serikali ya Marekani
kuzuia fedha za msaada kwa ajili ya maendeleo Millennium Challenge Cooperation
(MCC), msemaji kambi rasmi ya upinzani Waziri kivuli wa Wizara wa Mambo ya Nje Mch.
Peter Msigwa ametoa tamko la kuwataka Jumuiya ya Ulaya nayo kuzuia misaada kwa
serikali Tanzania iweze kujitafakari kama imezingatia vigezo vya MCC katika
kupata misaada.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika
ukumbi wa Hotel ya M. R, Mch. Msigwa ambaye pia ni Mbubge wa Jimbo la Iringa
Mjini alisema kambi ya upinzani imesikitishwa na maelezo ya Waziri wa Mambo ya
Nje Balozi Agustino Mahiga kutowaeleza wazi watanzania sababu hasa ya serikli
ya Marekani kusitisha utolewaji wa fedha hizo za msaada badala yake kukurupuka
na kutoa sababu ambazo hazina mashiko kwa wananchi.
Amesema kuwa sababu ambazo Balozi Mahiga
alizitoa juzi hazina mashiko kwa kuwa serikali ya Tanzania imekiuka misingi
mojawapo inayozingatiwa na MCC katika vigezo 17 katika kuchagua nchi
inayostahili kupata msaada na miongoni mwa vigezo vya msingi kabisa ni nchi
husika kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha demokrasia na kuendesha chaguzi
zilizo huru na haki.
Amesema kuwa katika taarifa yake MCC ilieleza
maeneo ambayo Tanzania imekiuka vigezo kuwa ni marudio ya uchaguzi haramu wa
urais Zanzibar na kupitisha Sheria ya Makosa ya Mawasiliano ya Mitandaoni
(Cyber Crime) sheria inayonyima uhuru wa wa kujieleza na uhuru wa kujumuika.
"Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za
kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika
utekelezwaji wa sheria ya Uhalifu wa Mtandao , Tanzania iliendelea na uchaguzi
wa marudio Zanzibar ambao haukushirikisha wote na wala haukuakisi maoni ya
wote, licha ya malalamiko kutoka kwa serikali ya Marekani na jamii ya
kimataifa”, amesema
Mchungaji Msigwa amesema kuwa kwa mantiki hiyo
ni dhahiri kuwa Tanzania haikupaswa kushitushwa na uamuzi wa MCC kwa kuwa
Serikali ilivifahamu vizuri na mapema vigezo vya kustahili kupewa misaada na MCC.
Aliongeza kuwa inashangaza na kusikitisha kuona
Msomi na Mwanadiplomasia mzoefu kama Balozi Mahiga akilitia Taifa Aibu ya Mwaka
kwa kulalamikia kuonewa na kutoa kauli za “hovyo” kama alivyozitoa.
Ameeleza kuwa kauli ya Waziri Mahiga, za
kukataa kukiri makosa yaliyo dhahiri yaliyofanywa na Serikali na Chama Chake
(CCM) zinaweza kabisa kuuweka rehani uhusiano na ushirikiano mzuri wa
kidiplomasia ambao Tanzania imekuwa ikiupata kutoka kwa nchi mbalimbali na
mashirika ya kimataifa kama MCC.
“Tukiweka mbele maslahi ya nchi hii yakiwemo ya
kudumisha mahusiano mazuri ya kimaendeleo na nchi nyingine, Kambi rasmi ya
Upinzani tunaiomba MCC, Marekani na mataifa mengine kuzipuuza kauli za hovyo
zilizotolewa na Waziri Mahiga, kwani haziakisi ustaarabu wa Watanzania” amesema
Mchungaji Msigwa.
Mchungaji Migwa ametaja sababu nyingine kuwa,
Tanzania si mbia mgeni kwa MCC na kusema kuwa Tanzania ilishapokea awamu ya
kwanza ya fedha za msaada kutoka MCC ambazo zilikuwa ni Dola za Marekani
milioni 698. Fedha hizi zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Tunduma-
Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.
Aidha amesema kuwa fedha hizo zilitumika pia
kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na
Morogoro na kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara na
nyingine zilitumika kutandaza njia ya
pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania
Visiwani na kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara
za Unguja kwa kiwango cha lami.
Pia amesema kuwa kwa namna yoyote ile
isingewezekana kwa MCC walewale kuionea Tanzania ile ile waliyoisaidia katika
awamu ya kwanza ya misaada yao na kwamba ni dhahiri kuwa Nchi imepoteza sifa
kwasababu zilizoelezwa – na kimsingi sababu zenyewe ni uchu na ulevi wa
madaraka uliopitiliza unaofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali
yake.
Amesema hatua ya MCC kusitisha uhusiano na
Tanzania ni ushahidi tosha kuwa hujuma za uchaguzi na ukiukwaji mkubwa wa
demokrasia na utawala bora, unaofanywa na serikali ya CCM na ambao Wapinzani
wamekuwa wakiulalamikia mara kwa mara sasa umefikia hatua mbaya zaidi kiasi cha
kugusa hisia za jumuiya ya kimataifa.
“Ni mtazamo wangu kuwa MCC na jumuiya ya
kimataifa bado walichelewa sana kugundua “udhalimu” wa Serikali ya CCM, ambayo
karibu mara zote imekuwa ikihujumu haki na uhuru wa watu kwenye chaguzi, na si
kwa upande wa Zanzibar tu, bali pia na uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano. Sheria
kandamizi zilizopo Tanzania si hiyo ya Cyber Crime tu. Tume ya Jaji Francis
Nyalali ilibainisha Sheria nyingi kandamizi na kushauri zifanyiwe mapitio ya
kuziboresha lakini hadi leo serikali isiyo ya kidemokrasia ya CCM imeendelea
kuzidumisha sheria hizo na kuongeza nyingine kama hii ya Cyber Crime. Natoa rai
kwa jumuiya ya kimataifa kutokukubali kurubuniwa tena na serikali ya CCM na
badala yake ishirikiane kwa karibu na Watanzania wote wazalendo katika
kuboresha misingi ya utawala bora na demokrasia kwenye nchi hii” amesema.
Pia alieleza sababu nyingine kuwa, mabalozi wa
nchi mbalimbali washirika wa maendeleo ikiwemo Marekani, walishatoa rai zaidi
ya mara moja wakiionya na kuishauri Serikali ya Rais Kikwete na baadaye Rais
Magufuli kuchukua hatua za kuutatua mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar na kwamba
walishauri mara kadhaa kuwa uchaguzi wa marudio usingeweza kuwa suluhu halali
ya kumaliza tatizo la Zanzibar na badala ya kuchukua hatua hasa za kukisihi
Chama chake kuheshimu maamuzi halali ya wapiga kura wa Zanzibar yaliyofanywa
Oktoba 25 mwaka jana na hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli,
alipuuza rai zote hizo.
“Mbali na Mabalozi hao, hata aliyekuwa Waziri
wa Mambo Nje wa Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe, alionya na kutoa
tahadhari kuhusu suala la Zanzibar lilivyokuwa likichukuliwa kwa mzaha-mzaha,
badala ya kutatuliwa kwa umakini na matokeo yake ndiyo haya ya kutengwa na MCC”
amesema.
Msigwa alionesha masikitiko yake kuwa Balozi
Mahiga anaingiza ukachero kwenye mambo ya msingi badala ya kuwaeleza watanzania
ukweli wa Marekani kusitisha fedha za MCC.
“Kwa asiyemjua Balozi Mahiga ni kachero mzoefu
wa siku nyingi tangu utawala wa Nyerere. Tunamtaka awaambie watanzania mambo ya
msingi siyo kuingiza ukachero. Tena aache mara moja.
“Serikali ya Tanzania ina imeweka watu wengine
kama hawana maana na kutumiwa vibaya. Haki za binadamu, watu wanateswa na
kunyanyaswa lakini Mahiga hayaoni na kuyasemea hayo na badala yake anawahadaa
watanzania” amesema.
Aidha alisema kuwa, wakati wa ubaguzi wa rangi
Afrika Kusini, Tanzania ilikuwa ya kwanza kuhamasisha nchi za kimataifa kuweka
vikwazo kwa sababu haki za binadamu zilikiukwa tena kwa makusudi lakini cha
kushangaza Tanzania hii hii imeingia katika ukiukaji wa haki za binadamu.
“Tunasikitishwa sana kwa kachero huyu kupotosha
wananchi. Ni wakati mwafaka wa Dkt. Mohamed Shein na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kukaa meza moja na kujitafakari.
“Kwa bahati mbaya nchi hii inaongozwa kwa
mwangwi. Watanzania wameaminishwa kuwa wamekusanya tunakusanya mapato mengi
sana! Serikali haijakataa fedha za MCC ila wanapotosha umma kwa kutoa sababu za
uongo. Tena watanzania wajue kuwa serikali haina uwezo wa kujitegemea” amesema.
No comments:
Post a Comment