BINADAMU anaelezwa kuwa ni kiumbe
kilichochafuka na uchafu wa kutisha ambao anahitaji msaada kwa ajili ya
kusafishwa.
Haya yamezungumzwa na Rais wa Baraza la
Maaskofu Tanzania Mhashamu askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alipokuwa akihubiri
katika Mkesha wa Pasaka Parokia ya Bikira Maria Consolata - Mshindo Jimbo la
Iringa.
Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni
askofu wa jimbo la Iringa alisema binadamu amejaa maovu ya kila aina ambayo
yamekuwa kikwazo kwa wengine na kusema kuwa bila nguvu ya Mungu mwanadamu pekee
hayawezi.
"Kristo amekuja kututoa katika
uhuni, ufisadi, unyang'anyi na dhuruma. Maovu yetu tuliyo nayo yanatokana na
ukaidi wetu na kiburi. Amebeba dhambi zetu akafa msalabani kwa ajili ya
kutukomboa utumwani mwa shetani.
"Tumejipaka mavi, mikojo na uchafu
wa kila aina. Tumejaa uchafu hata tumekuwa kinyaa, hatutamaniki kwa wengine.
Sasa tumekombolewa kwa damu ya mwana kondoo" amesema.
Amesema mwanadamu ameingia mkataba wa
urafiki na ibilisi na kumfanya kikaragosi wake kumtumikisha katika dhambi na
kwamba muda wa kuufuta mkataba huo umefika.
Ameasa kuwa manyanyaso ya mwanadamu
yanayotokana na ukaidi na kiburi kutopenda kutii maagizo ya Mungu kutenda mema.
Hata hivyo alisema mwanadamu ana deni
kubwa kurudi kwa Mungu na kuachana na matendo yanayomchukiza Mungu kwa
kuwapendeza wanadamu wenzake, kuachana na ufisadi na matendo yote yasiyo ya
haki.
No comments:
Post a Comment