TATIZO la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Albino linalozidi kushika kasi nchini Tanzania linaelezwa kuwa linatokana na watu wenye uchu wa madaraka na mali ambao wamekosa maadili na hofu ya Mungu huku wanasiasa wakihusishwa na jambo hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mtandao huu, wananchi wanaoneshwa kusikitishwa na vitendo hivyo huku wakiitupia
lawama serikali kuwa inaonesha uzembe wa makusudi kulichukulia uzito suala
hilo.
Sisto Khani mkazi wa Iringa mjini
ameuambia mtandao huu kuwa, serikali imeonesha udhaifu katika suala hili
kutokana na kutowachukulia hatua kali watuhumiwa wanaokamatwa kwa vitendo hivyo
na kwamba kama serikali itaendelea kuonesha udhaifu wa namna hiyo, vitendo
hivyo haviwezi kuisha.
Hata hivyo Sisto alisema pamoja na
serikali kuonesha udhaifu katika suala hilo, ushirikina ndio chanzo kikubwa cha
vitendo hivyo kutokana na watu kuamini kuwa kwa kutumia viungo vya watu hao unaweza
kupata utajiri au kutimiza matakwa yao.
“Ushirikina na chanzo cha mauaji ya
albino kwa sababu kuna watu wanatumia njia hiyo eti wanataka vyeo, utajiri,
mali na uongozi” amesema.
Amesema kuwa wanasiasa ndio watuhumiwa
wakubwa kutokana na vitendo hivyo kufanyika zaidi wakati wa chaguzi.
“Mauaji mengi ya albino yanatokea zaidi
unapokaribia uchaguzi. Tunakumbuka mauaji haya yalitokea sana mwaka 2010 lakini
angalia mwaka huu wa uchaguzi mauaji yameibuka upya. Ni dhahiri wazi kuwa hawa
wanasiasa hawa wanafanya hivyo wakiamini kuwa hawawezi kutoka madarakani.
“Serikali haijatenda haki hata kidogo
kwa sababu hatujaona watuhumiwa wakihukumiwa au wakinyongwa licha ya kuwa
tunasikia tu kuwa wamekamatwa. Wangenyongwa nadhani lingekuwa fundisho kwa
wengine lakini kwa sababu tatizo ni wale wanaojulikana ndiyo maana serikali
haifanyi hivyo” amesema.
Kwa upande wake Asha Hingi mkazi wa mtaa
wa Kinyanambo “A” Mafinga, akiongea na mtandao huu nyumbani kwake amesema
licha ya kuwa Mafinga haina albino wengi, vitendo wanavyotendewa ni vya
kishetani ambavyo vinatakiwa kutofumbiwa macho na mtu yeyote.
Amesema kuwa jamii inapaswa kulitambua
hili na kufanya ulinzi wa hali ya juu kuwabaini wauaji hao na kuwashughulikia
ipasavyo kwani vitendo wanavyofanya si vya kiungwana.
“Vitendo hivi ni vya kusikitisha sana
tena ni aibu kwa taifa letu kusifika kwa mauaji ya wenzetu! Kila mtu anapaswa
kuwatambua hawa albino kuwa ni watu kama tulivyo wengine na wanapaswa kupata
haki zote ambazo sisi tunazipata na tunazihitaji.
“Pia jamii inapaswa kuhakikisha inawajibika
kwa dhati katika kuhakikisha usalama wa watu hawa. Kwa nini hawa wenzetu waishi
kama wakimbizi? Jaamani watanzania tuwe na huruma kwa wenzetu hawa".
Ameitaka jamii kutokupuuza suala na
kutaka kula mtu kulichukulia uzito kama nake kwa kuwa kuzaa albino kunaweza kumpata
mtu yeyote wakati wowote bila yeye kutarajia.
Pamoja na kuvihusisha vitendo hivyo na
masuala ya ushirikina, ameitaka jamii pale anapozaliwa albino katika familia
kuliweka wazi jambo hilo ili jamii ijue
na kusaidia ulinzi badala ya kuficha na kuhatarisha maisha ya familia.
Kalinga Mawazo mkazi wa Mafinga, naye
anawashutumu vikali wafanyabiashara na wanasiasa kuwa wao ndicho chanzo kikubwa
cha mauaji ya albino akiwahusisha kushiriki vitendo vya kishirikina.
“Hatujajua kama kweli ni siasa lakini
wanasiasa na wafanyabiashara wanaweza kuwa chanzo kikubwa kwa sababu ya
masharti yao ya ushirikina wakiamini kuwa wataendelea kibiashara na na
wanasiasa kuamini kuwa hawatapoteza nafasi zao za uongozi kitu ambacho waganga
wanaowatumia wanawadanganya” amesema.
Mtandao huu umefanikiwa kupiga hodi kwa
mzee mmoja anayeaminika kuwa ni mganga wa jadi ambapo lilifanikiwa kufanya
mahojianao kwa masherti ya kutotaka jina liandikwe.
Akitoa maelezo kwa masharti hayo,
alikiri kuwapo kwa vitendo hivyo na kwamba ni kweli wapo baadhi ya watu
wanaojiita waganga kutaka viungo vya watu kama hao kwa madai kuwa ni mazindiko
huku wakidanganya watu.
“Ni kweli vitendo hivi vipo sana na
vinanisikitisha sana. Kuna baadhi ya watu wanajiita waganga wanadanganya watu
kuwa wanawazindika na kuwataka wakalete vitu kama hivyo lakini watu wenyewe
bila kufikiria wanakwenda kuwaua wenzao bila huruma.
“Hata mimi ninachojiuliza ni kwamba, ina
maana hawa wanaojiita waganga wenye tabia hizo, wakizaliwa albino katika
familia zao watawaua? Nawaomba watu wasikubali kudanganywa na watu kama hao kwa
sababu ni uongo mkubwa. Halafu naiomba serikali kuwanyonga watu wanaojifanya
waganga wa mtindo huo kwa sababu wanatudhalilisha sisi wengine” kimesema chanzo
chetu.
Hata hivyo chanzo hicho kilipotakiwa kuwataja watu hao wanaosadikiwa waganga wanaojihusisha na vitendo hivyo
kwa kuwadanganya watu, kilisema hakina majina.
“Sina majina ya watu kama hao ila
naamini kuwa vitendo hivi vipo na vinafanyika na baadhi ya watu wanaotumia jina
la uganga kwa ajili ya kutafuta pesa japo kuwa hata mimi sijawafahamu kwa
sababu kwenye maeneo yetu hakuna matukio ya kikatili kama hayo” kimesema chanzo
chetu.
Mwaka 2010 serikali ililazimika kuwataka
wananchi kupiga kura kubaini wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya albino na
ujambazi jambo lililofanyika japo kuwa majibu ya kura hizo hayakutolewa hadi
leo.
No comments:
Post a Comment