Wakenya sita waliokuwa wamefunguliwa
mashtaka na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) kuhusiana
na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 wamekusanyika kwa mkutano wa
maombi mjini Nakuru kusherehekea kutamatishwa kwa kesi dhidi ya Naibu
Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Sang.
Mji wa Nakuru unapatikana katika uliokuwa mkoa wa Bonde la Ufa na uliathirika sana wakati wa mapigano hayo.
Rais Uhuru Kenyatta, aliyekuwa miongoni mwa waliofunguliwa mashtaka, amekuwa akihimiza maridhiano na umoja.
Wengine
waliokuwa wamefunguliwa mashtaka ni aliyekuwa mkuu wa polisi Meja
Jenerali Hussein Ali, aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma Francis
Muthaura na waziri wa zamani Henry Kosgey.
Watu takriban 1,300 walifariki na wengine 600,000 wakafurushwa makwao, wengi wao eneo la Bonde la Ufa, wakati wa mapigano hayo.
Mahakama ya ICC awali ilithibitisha mashtaka dhidi ya Bw Kenyatta, Bw
Ruto na Bw Sang lakini kesi dhidi ya Bw Kenyatta ikaondolewa Desemba
mwaka 2014.
Kesi dhidi ya Bw Ruto na Bw Sang ilitamatishwa na majaji mapema mwezi huu.
Mwendesha
mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC Fatou Bensouda alikuwa amelalamika
kwamba mashahidi wengi wamehongwa au kutishwa na wakabadilisha ushahidi
waliokuwa wametoa awali na wengine wakajiondoa.
- Ruto: Waathiriwa wa ghasia lazima wapate haki
- Bensouda: Kenya haikushirikiana na ICC
- Ruto ashinda rufaa mahakama ya ICC
Wakati wa kutamatisha kesi dhidi ya Bw Ruto na Bw Sang tarehe 5
Aprili, Jaji Chile Eboe-Osuji kwenye uamuzi wake alisema huenda
kuingiliwa kwa mashahidi kulidhoofisha kesi hiyo.
Aidha, alisema kulikuwa na uingiliaji wa kisiasa ambao huenda uliwatia hofu baadhi ya mashahidi.
Wiki hii, mjadala kuhusu kesi hizo umefufuliwa tena baada ya kiongozi
wa upinzani Raila Odinga kukosoa hatua ya ICC kutamatisha kesi dhidi ya
viongozi wakuu Kenya.
Alisema hilo huenda likawafanya viongozi na wanasiasa Afrika kutozingatia mfumo wa sheria wanapotawala.
Bw
Odinga alidai kwenye mahojiano na shirika la habari la AFP kwamba
kutokana na uamuzi huo wa ICC, viongozi wengi wa kiafrika watakuwa
madikteta na hawataogopa kushtakiwa na ICC kwa vile wanaweza
kuhitilafiana na ushahidi bila kujali madhara yake.
Bw Kenyatta na
Bw Ruto wakijibu madai hayo kwenye mkutano wa hadhara eneo la
Nyandarua, katikati mwa Kenya, walimshutumu Bw Odinga wakisema alitaka
kujifaidi kisiasa kupitia kesi hizo.
Hisia miongoni mwa Wakenya zimegawanyika baadhi wakisema kuna haki ya kusherehekea kutamatishwa kwa kesi dhidi ya Wakenya hao.
Kuna wengine hata hivyo
wanaoamini kwamba si haki kusherehekea ikizingatiwa kwamba wengi wa waathiriwa wa ghasia hizo bado wanateseka.
Kwenye Twitter, mgawanyiko huo unajitokeza wazi kukiwa na vitambulisha mada vinavyoshindana.
Wanaounga
mkono mkutano huo wa Afraha, Nakuru na kuhimiza maridhiano wanatumia
kitambulisha mada #WeAreOneAfraha (Sisi tuna umoja Afraha) na
#UhuruRutoThanksgiving (Ibada ya kutoa shukrani ya Uhuru na Ruto).
Wanaotetea waathiriwa, kuna kitambulisha mada cha #WhatAboutTheVictims (Na Waathiria hatima yao gani).
Chanzo: bbc swahili
No comments:
Post a Comment