Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje Mch. Peter Msigwa akiongea na waandishi wa habari juu ya fedha za MCC. |
SIKU chache baada ya Serikali ya Marekani
kuzuia fedha za msaada kwa ajili ya maendeleo Millennium Challenge Cooperation
(MCC), msemaji kambi rasmi ya upinzani Waziri kivuli wa Wizara wa Mambo ya Nje Mch.
Peter Msigwa ametoa tamko la kuwataka Jumuiya ya Ulaya nayo kuzuia misaada kwa
serikali Tanzania iweze kujitafakari kama imezingatia vigezo vya MCC katika
kupata misaada.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika
ukumbi wa Hotel ya M. R, Mch. Msigwa ambaye pia ni Mbubge wa Jimbo la Iringa
Mjini alisema kambi ya upinzani imesikitishwa na maelezo ya Waziri wa Mambo ya
Nje Balozi Agustino Mahiga kutowaeleza wazi watanzania sababu hasa ya serikli
ya Marekani kusitisha utolewaji wa fedha hizo za msaada badala yake kukurupuka
na kutoa sababu ambazo hazina mashiko kwa wananchi.
Amesema kuwa sababu ambazo Balozi Mahiga
alizitoa juzi hazina mashiko kwa kuwa serikali ya Tanzania imekiuka misingi
mojawapo inayozingatiwa na MCC katika vigezo 17 katika kuchagua nchi
inayostahili kupata msaada na miongoni mwa vigezo vya msingi kabisa ni nchi
husika kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha demokrasia na kuendesha chaguzi
zilizo huru na haki.
Amesema kuwa katika taarifa yake MCC ilieleza
maeneo ambayo Tanzania imekiuka vigezo kuwa ni marudio ya uchaguzi haramu wa
urais Zanzibar na kupitisha Sheria ya Makosa ya Mawasiliano ya Mitandaoni
(Cyber Crime) sheria inayonyima uhuru wa wa kujieleza na uhuru wa kujumuika.
"Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za
kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika
utekelezwaji wa sheria ya Uhalifu wa Mtandao , Tanzania iliendelea na uchaguzi
wa marudio Zanzibar ambao haukushirikisha wote na wala haukuakisi maoni ya
wote, licha ya malalamiko kutoka kwa serikali ya Marekani na jamii ya
kimataifa”, amesema
Mchungaji Msigwa amesema kuwa kwa mantiki hiyo
ni dhahiri kuwa Tanzania haikupaswa kushitushwa na uamuzi wa MCC kwa kuwa
Serikali ilivifahamu vizuri na mapema vigezo vya kustahili kupewa misaada na MCC.
Aliongeza kuwa inashangaza na kusikitisha kuona
Msomi na Mwanadiplomasia mzoefu kama Balozi Mahiga akilitia Taifa Aibu ya Mwaka
kwa kulalamikia kuonewa na kutoa kauli za “hovyo” kama alivyozitoa.