KLERUU

KLERUU
KLERUU

Ibada

Ibada

Saturday, February 27, 2016

Rushwa yabadilishwa jina sasa yaitwa "mipango"


WAKATI Serikali ya awamu ya tano ikija na neon utumbuaji majipu, baadhi ya watendaji wamekwepa kuita rushwa au takrima na kubuni jina linguine kuwa ni “mipango”.

Mtandao huu umeshuhudia baadhi ya maofisa watendaji wakitaka kupa fedha kutoka kwa mwanamke mmoja aliyekuwa akijenga kiti cha nyumba katika mtaa wa Igumbilo Kata ya Ruaha katika Manispaa ya Iringa wakidai kuwa za mipango.

Wakati watendaji hao wakimkomalia mwanamke huyo ili awapatie fedha, walikuwa wakitumia kigezo kuwatamsimamisha asiendelee na ujenzi kwa sababu ya kutokuwa na kibali.

Wakati wakiendelea kumkomalia mama huyo mtandao huu ulitaka kujua kama hizo fedha ambazo angezitoa mama huyo zinatolewa stakabadhi na kama ni za kisheria lakini ofisa mtendaji wa mtaa huo Ashery Msigala alisisitiza kuwa ni kwa ajili ya mipango.

“Siku zote ukitaka kufanikiwa kwa haraka lazima uwe na mipango. Ukitaka kufanyiwa kazi yako kwa haraka zaidi lazima uwe na mipango.

“Unapoamka kwenda ofisi ya mtu kwa ajili ya kupata huduma, ili huduma hiyo iweze kwenda kwa haraka zaidi lazima unapoondoka uwe na mipango kama hamasa kwa mtendaji unayekwenda kuonana naye ili akusaidie” amesema Msigala.



Mtandao huu ulipotaka kupata ufafanuzi zaidi maana ya mipango, mtendaji huyo alisema ni ile hamasa inayomfanya mtu kutoa huduma kwa haraka zaidi.

Hata hivyo Msigala alisisitiza kuwa siyo rushwa ila ni mipango inayofanikisha shughuli kwa haraka zaidi kuliko.

“Unaweza ukatenga hata elfu mbili tu kwa ajili ya kumpa mtoa huduma ili iwe hamasa kwake akusaidie kwa haraka zaidi kwa sababu mnaohitaji huduma kama hiyo ni wengi kwa hiyo akikuweka katika foleni utachelewa kwa hiyo ukimpa hata buku mbili inamhamasisha afanye kazi kwa haraka zaidi. Ila hii siyo rushwa ni mipango tu unayojiwekea kwa ajili ya kazi zako ziweze kwenda kwa wakati” amesema Msigala.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kwa kile kilichoelezwa kuwa angeweza kusimamishwa asiendelee kujenga, mwanamke huyo alieleza kuwa aliandika barua ya kuomba kibali kwa ajili ya kuanza ujenzi ikapitishwa kwa ofisa mtendaji wa mtaa akaona majibu ya kibali yanachelewa akaamua kuanza ujenzi.

Alipoulizwa mbele ya mtendaji huyo kama barua hiyo ilipitia kwake, mwanamke huyo alionesha wazi kuwa aliipokea mtendaji huyo mkononi.

“Niliandika barua nikampa mtendaji huyu (akimuonesha Msigala) akaisaini akasema kuwa ataipeleka Manispaa ili wanipe kibali lakini tangu niandike barua hiyo ni mwezi umepita sijapata majibu nikaamua kuanza sasa nashangaa anaposema ananisimamisha” amesema mama huyo.

Alipotakiwa kuthibitisha kuwa alipokea barua ya mama huyo, Ashery Msigala alikiri kuwa aliipokea na kwamba majibu yanachelewa kutoka Manispaa.

“Nilipeleka Manispaa Barua yake ila majibu yanachelewa na tumekuja kumsimamisha kwa sababu kuna watu wanatuuliza kuwa kwa nini huyu mama anajenga bila kibali! Na kibali kinachelewa kwa sababu kama nilivyosema awali hakuna mipango” amesema Msigala.

Wakazi wa mtaa huo wamesema ni kawaida kwa mtendaji huyo kupita na kuomba fedha kwa sababu ya mipango ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment