|
Wakenya hao wamesisitiza kwamba hawakuhusika katika ghasia hizo
|
Wakenya sita waliokuwa wamefunguliwa
mashtaka na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) kuhusiana
na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 wamekusanyika kwa mkutano wa
maombi mjini Nakuru kusherehekea kutamatishwa kwa kesi dhidi ya Naibu
Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Sang.
Mji wa Nakuru unapatikana katika uliokuwa mkoa wa Bonde la Ufa na uliathirika sana wakati wa mapigano hayo.
Rais Uhuru Kenyatta, aliyekuwa miongoni mwa waliofunguliwa mashtaka, amekuwa akihimiza maridhiano na umoja.
Wengine
waliokuwa wamefunguliwa mashtaka ni aliyekuwa mkuu wa polisi Meja
Jenerali Hussein Ali, aliyekuwa mkuu wa utumishi wa umma Francis
Muthaura na waziri wa zamani Henry Kosgey.
Watu takriban 1,300 walifariki na wengine 600,000 wakafurushwa makwao, wengi wao eneo la Bonde la Ufa, wakati wa mapigano hayo.
|
Wakenya sita walikuwa wamefunguliwa mashtaka ICC
|
Mahakama ya ICC awali ilithibitisha mashtaka dhidi ya Bw Kenyatta, Bw
Ruto na Bw Sang lakini kesi dhidi ya Bw Kenyatta ikaondolewa Desemba
mwaka 2014.
Kesi dhidi ya Bw Ruto na Bw Sang ilitamatishwa na majaji mapema mwezi huu.
Mwendesha
mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC Fatou Bensouda alikuwa amelalamika
kwamba mashahidi wengi wamehongwa au kutishwa na wakabadilisha ushahidi
waliokuwa wametoa awali na wengine wakajiondoa.
Wakati wa kutamatisha kesi dhidi ya Bw Ruto na Bw Sang tarehe 5
Aprili, Jaji Chile Eboe-Osuji kwenye uamuzi wake alisema huenda
kuingiliwa kwa mashahidi kulidhoofisha kesi hiyo.
Aidha, alisema kulikuwa na uingiliaji wa kisiasa ambao huenda uliwatia hofu baadhi ya mashahidi.