NA MWANDISHI WETU, NJOMBE.
RAIA mmoja mkazi wa Njombe mjini ameuawa
kwa risasi na Polisi kitendo kilichowatia hasira wananchi na kufunga mitaa kwa
maandamano mkoani Njombe kwa kutaka kujua sababu zilizowafanya Polisi kufyatua
risasi kwa wananchi na kusababisha kifo cha mwanachi huyo.
Kutokana na tukio hilo wananchi waliamua
kufanya maandamano leo kutaka kujua sababu za mwezao kuuawa jambo
lililosababisha jeshi la polisi kutumia mabomu na silaha za moto hapo na
kujeruhi raia wengine wawili katika maandamano hayo.
Hasira za wananchi hao zimesababisha
shughuli kusimama kwa siku nzima huku maduka yakifungwa pamoja na usafiri kuwa
mgumu kutokana na wananchi kutaka kupata majibu ya kuuawa kwa raia huyo.
Wakizungumza na mtandao huu,
wananchi wakazi wa Njombe wamesema Polisi walifika kilabuni walikokuwa wakinywa
pombe wananchi na kufyatua risasi bila sababu yoyote kisha kumpiga mwananchi
huyo aliyefariki dunia papo hapo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Amos
Nziku ameeleza kuwa, ilikuwa majira ya jioni jana walipokuwa wakipata vinywaji
katika kilabu kimoja cha pombe ambapo alitokea raia mmoja akaingia kilabuni
hapo akikimbia jambo lililowashtusha na kumtaka kueleza sababu ya kuingia akiwa
anakimbia.
“Jana tulikuwa kilabu cha Nyondo
tukipata kiburudisho chetu cha koo huku tukiongea na marafiki gafla akaingia
mtu akikimbia tukashtuaka sana. Sasa kule kushtuka kila mtu akataka kujua
anakimbia nini, yule jamaa akatuambia polisi wanamfukuza.
“Tulitoka watu wote pale kilabuni
kuangalia tukawaona kweli polisi tukaanza kuwapigia kelele kutaka kujua ni kwa
nini wanamfukuza. Lengo ni kujua kama ni mwizi ili tumshughulikie lakini cha
kushangaza, polisi wakaanza kufyatua risasi kuelekeza kwetu. Kwa bahati mbaya
risasi ilimfikia mwenzetu mmoja akafariki papo hapo” amesema Nziku.
Hata hivyo Emelia Sanga ameliambia mtandao huu kuwa imekuwa ni kawaida kwa polisi wa Njombe kutaka hela kwa nguvu
kutoka kwa wananchi na kwamba inaonesha kumfukuza raia huyo hadi kukimbia
kilabuni walikuwa wakimtaka hela.
“Njombe polisi wanatutesa na kama ndivyo
wanavyofundishwa huko wanakojifunza upolisi basi nchi hii wataishi wenyewe.
Wamekuwa wakisumbua watu kwa kuwataka hela kwa nguvu. Inaonesha hata huyu
waliyekuwa wanamfukuza walikuwa wanataka hela akawa anakimbia. Maana hawa jamaa
ukiona umesimama tu unalo! Na hivi alikuwa na gari wangemuandikia kosa lolote
hata kama hana kosa.
“Kweli nasikitika sana kwa sababu zamani
enzi za Mwalimu tukiwaona polisi tulikuwa na amani lakini kwa siku hizi
tukiwaona hawa jamaa ni afadhali tuwaone simba. Hawa jamaa wamekuwa ni zaidi ya
wanyama tena wakionekana sehemu tunawakimbia kabisa” amesema Sanga.
Akizungumza na mtandao huu kwa masharti
ya kutotaka jina lake liandikwe kwa kuwa yeye si msemaji, mmoja wa jeshi la
polisi Mkoa wa Njombe amesema kuwa wakati wakifanya doria waliliona gari ambalo
walilitilia mashaka na kuanza kulifuatilia ambapo mwenye gari baada ya kugundua
kuwa tunamfuatilia alikwenda kuingia kilabuni na kuwatoa wananchi wakiwa na
hasira wakaanza kutupigia kelele na kuturushia mawe lakini katika kujihami
tukatumia silaha za moto.
“Jana tulikuwa doria na gari la kiraia lakini
tukiwa katika shughuli hiyo tukaliona gari kwenye kituo cha mafuta gari ambalo
tulilitilia shaka tukasimama ili kuona linaelekea wapi. Baada ya kuondoka pale
kwenye kituo cha mafuta badala ya kuingia katika barabara kubwa likaingia
barabara za uchochoroni ndipo tulipoanza kulifuatilia linakokwenda.
“Inaonekana Yule dereva alitugundua
halafu akafika katika kilabu kimoja kinaitwa Nyondo akasimamisha gari lake
halafu akatoka mbio akakimbilia mule ndani. Baada ya kuingia dakika chache tu
tukaona wengi wanatoka wakiwa na hasira huku wakiturushia mawe na kupiga
mayowe. Katika kujihami tukaanza kufyatua risasi hewani ili watawanyike kisha
tukaondoka lakini kwamba tumeua hilo mimi sijui kama kweli tumemua sisi”
kimesema chanzo chetu.
Hata hivyo chanzo hicho kilipotakiwa
kueleza kuwa walikuwa na shaka gani juu ya gari hilo kimesema ni kiintelijensia
zaidi na kwamba haiwezekani kusema kwa kuwa ni za kiusalama na ni shughuli za kipolisi.
Mtandao huu ulipomtafuta kamanda wa
Polisi Mkoa wa Njombe Franco Kibona ili kutolea ufafanuzi juu ya suala hilo alisema hawezi kuzungumza chochote
kwa kuwa yupo kwenye kikao na kwamba hali ya usalama haijakaa vizuri.
No comments:
Post a Comment