NA MWANDISHI WETU, NJOMBE.
RAIA mmoja mkazi wa Njombe mjini ameuawa
kwa risasi na Polisi kitendo kilichowatia hasira wananchi na kufunga mitaa kwa
maandamano mkoani Njombe kwa kutaka kujua sababu zilizowafanya Polisi kufyatua
risasi kwa wananchi na kusababisha kifo cha mwanachi huyo.
Kutokana na tukio hilo wananchi waliamua
kufanya maandamano leo kutaka kujua sababu za mwezao kuuawa jambo
lililosababisha jeshi la polisi kutumia mabomu na silaha za moto hapo na
kujeruhi raia wengine wawili katika maandamano hayo.
Hasira za wananchi hao zimesababisha
shughuli kusimama kwa siku nzima huku maduka yakifungwa pamoja na usafiri kuwa
mgumu kutokana na wananchi kutaka kupata majibu ya kuuawa kwa raia huyo.
Wakizungumza na mtandao huu,
wananchi wakazi wa Njombe wamesema Polisi walifika kilabuni walikokuwa wakinywa
pombe wananchi na kufyatua risasi bila sababu yoyote kisha kumpiga mwananchi
huyo aliyefariki dunia papo hapo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo Amos
Nziku ameeleza kuwa, ilikuwa majira ya jioni jana walipokuwa wakipata vinywaji
katika kilabu kimoja cha pombe ambapo alitokea raia mmoja akaingia kilabuni
hapo akikimbia jambo lililowashtusha na kumtaka kueleza sababu ya kuingia akiwa
anakimbia.
“Jana tulikuwa kilabu cha Nyondo
tukipata kiburudisho chetu cha koo huku tukiongea na marafiki gafla akaingia
mtu akikimbia tukashtuaka sana. Sasa kule kushtuka kila mtu akataka kujua
anakimbia nini, yule jamaa akatuambia polisi wanamfukuza.
“Tulitoka watu wote pale kilabuni
kuangalia tukawaona kweli polisi tukaanza kuwapigia kelele kutaka kujua ni kwa
nini wanamfukuza. Lengo ni kujua kama ni mwizi ili tumshughulikie lakini cha
kushangaza, polisi wakaanza kufyatua risasi kuelekeza kwetu. Kwa bahati mbaya
risasi ilimfikia mwenzetu mmoja akafariki papo hapo” amesema Nziku.