Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo Zitto Kambwe akiwahutubia wakazi wa Manispaa ya Iringa |
KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo
Zitto Kabwe amesema Chamani cha Mapinduzi kinashindwa kutofautisha uongozi wa
chama na uongozi wa serikali na kusababisha kuwafanya wananchi kushindwa kujua
utendaji wa viongozi hao.
Zitto ameyasema hayo alipokuwa
akiwahutubia wakazi wa Manispaa ya Iringa katika Mkutano wa chama hicho
uliofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa.
Amesema si rahisi kujua utendaji wa kazi
za chama na kazi sa serikali kwa Rais Jakaya Kikwete kutokana na kuwa na kofia
mbili za uenyekiti wa chama taifa na kofia ya urai wan chi na kwamba
haijulikani ni wakati gani anafanya kazi za chama na ni wakati gani anafanya
kazi cha taifa.
Amesema nchi inakosa mwelekeo kutokana
na kuwapo kwa mfumo wa uongozi wa kinyonyaji na dhuruma unaotokana na viongozi
wasiokuwa na maadili ambao kazi yao ni kufanya unyonyaji badala ya kufanya kazi
za taifa.
“Ifike mahali ikaeleweka na kutofautisha
viongozi wa chama na viongozi wa serikali ili utendaji uweze kueleweka. Si
rahisi kutambua Rais Kikwete ni wakati gani anafanya kazi za chama na ni wakati
gani anafanya kazi za taifa.
“Mfumo wa uongozi wa namna hii ni wa
kinyonyaji kwa kuwa viongozi wengi wanafanya kazi za kinyonyaji kwa kuwa hakuna
wa kumkemea mwenzake. Ndiyo maana hata mafisadi wanatazamwa usoni tu kwa sababu
mfumo wa uongozi ndivyo ulivyo” amesema.
Amesema mtu yeyote akisema yeye ni
kiongozi lazima awe mpambanaji kupigania haki za watu wake kwa ajili ya
kuhakikisha watu wake wanakuwa na maendeleo.
Amesema umasikini wa watanzania
unasababishwa na wabunge wasiopamba kupigania haki za watu wao na kugeuka kuwa
wanyonyaji wasio na huruma.
Amewataka watanzania kuwa kuelewa kuwa
si kwamba ufisadi unakwisha bali unaendelea kwa kasi zaidi kwa kuwa serikali
iliyopo madarakani imekosa meno kuwashughulikia wezi sugu wanaoiba mali ya umma
na kwamba umasikini ni chaguo la viongozi wa kisiasa.
“Umasikini wa Tanzania ni chaguo la
viongozi wa kisiasa. Tusipofanya mabadiliko sisi wananchi, umasikini huu
utaendelea kuwapo na hautakoma kwa kuwa wenzetu wa chama tawala ndio chaguo
lao” amesema.
Amesema tatizo kubwa uchumi umeshikiliwa
na watu wachahe ambao hao hao ni viongozia wa kisiasa na wengine ni viongozi wa
serikali na kwamba uchumi wa Iringa pia umeshikiliwa na watu wa namna hiyo.
Pia amewataka wananchi kutokubali
kukodishiwa ardhi na wawekezaji kwa kuwa ardhi ni mali ya watanzania kwa matumizi
ya maendeleo ya watanzania na taifa lao.
Katika hatua nyingine Zitto ameshangazwa
na kitendo cha watuhumiwa wa wizi wa fedha za Tegeza Escrow kupewa ujenzi wa
bandari ya Mwambani jijini Tanga bila kuwapo kwa tangazo la zabuni ya ujenzi wa
bandari hiyo.
“Tunamtaka Waziri wa uchukuzi Samwel
Sitta afanye uchunguzi wa ujenzi wa bandari ya Mwambani kule Tanga na aueleze
umma zabuni ya ujenzi huo ilitangazwa lini! Cha kushangaza zaidi waliopewa kazi
ya ujenzi wa bandari hiyo ni wale watuhumiwa wa wizi wa fedha za Escrow. Hili
la kuwapatia mafisadi wa Escrow ujenzi wa bandari halikubaliki hata kidogo”
amesema.
Amesema watanzania watambue kuwa vitendo
vyote vinavyofanyika nchini na kuwaumiza wananchi vinatokana na viongozi kukosa
miiko ya uongozi ambayo ipo wazi katika Azimio la Arusha.
“Labda niwakumbushwe watanzania
mnaolijua Azimio la Arusha na niwaambie msiolijua Azimio hili kuwa, katika
Azimio la Arusha kuna mambo makubwa manne ambayo ni msingi wa Azimio zima.
Jambo la kwanza ni Siasa ya Ukombozi, jambo la pili ni Siasa ya Kujitegemea,
Jambo la tatu ni Madhumuni ya TANU na jambo la nne ni Miiko ya Uongozi.
“Haya yote hawa viongozi wenzetu
wameyatupilia mbali na ndiyo maana kumekithiri kwa vitendo vya kifisadi kwa
sababu hawana maadili hawa wanaojiita viongozi. Ni lazima turudi kwenye misingi
ya nchi hii, ni lazima kila Mtanzania awe katika uchumi wa nchi hii” amesema.
Pia amesema, ili kurejesha miiko ya
uongozi na misingi ya taifa hili ni lazima viongozi kuweka wazi mali walizo
nazo ili wananchi waweze kujua na kuzitambua badala ya kuficha na kuendelea
kuiba na kujilimbikizia.
Hata hivyo Zitto amemtaka Rais Kikwete
kuunda bunge maalumu la Katiba ili lifanye mapitio ya rasimu ya Tume ya Katiba
iliyoandaliwa na Jaji Warioba ili maoni ya wananchi yasipuuzwe kama ilivyofanyika
Dodoma wakati wa Bunge maalumu lililoiweka pembeni rasimu ya hiyo na
kutengeneza maoni yao.
Hata hivyo Zitto amesema watanzania
wanapaswa kumpima kwa matendo yake badala ya kumpima kwa maneno ili mwisho wa
kipimo hicho waweze kupata majibu sahihi.
“Ninajua kuwa kuna propaganda nyingi tu
ila kwa kuwa mimi ni mwanasiasa hazinisumbui. Ukiwa mwanasiasa lazima uwe na
ngozi ngumu. Ninachowaomba wananchi, nipimeni kwa matendo yangu, msinipime kwa
maneno ya wapinzani wangu, kaeni mtupime, wekeni wabunge wote mtapata majibu ni
nani mnyonge mwenzenu, ni nani anayewatetea, ni nani mnayetaka kumtetea na ni
nani mnatembea pamoja” amesema.
Wakati Zitto akiomba wananchi wampime
kwa matendo yake, wananchi wamekuwa na maswali kuwa ni matendo gani anayasema
ikiwa inajulikana kuwa yeye ni msaliti na akionesha kuwa na uchu wa madaraka.
Kwa nyakati tofauti wananchi wamesikika
wakijadili vijiweni kuwa hawaoni matendo ya kumpima Zitto zaidi ya tendo la
usaliti alilolifanya na kuhoji kuwa ikiwa ni uzalendo anaotaka kuufanya ni kwa
nini hakutaka kuufanya akiwa ndani ya chama alichokisaliti.
Pascal Madafu mkazi wa Kihesa ni
miongoni mwa wananchi wanaomshangaa Zitto kwa kutaka apimwe kwa matendo yake
yepi!
“Hivi Zitto anayemdanganya ni nani?
Tunachokijua hadi sasa ni kwamba yeye ni msaliti sasa nimeshangaa anaposema
tumpime kwa matendo yake. Ni matendo gani anayotaka tumpime? Matendo ya usaliti
au ni nini hasa?
“Kingine ambacho tunaelewa ni kwamba
yeye alishaonekana mapema kuwa ana uchu wa madaraka. Hapa anatafuta umaarufu tu
lakini hakula lolote. Asije akawa kipandikizi kwa ajili ya kuvuruga nguvu ya
upinzani kama ilivyofanyika mwaka 1995. Tunayakumbuka sana na lazima tuwe
makini na watu kama hawa. Ni mapema mno kusema Zitto anafaa kwa sababu tusije
tukajiloga wenyewe” anasema Madafu.
Nziku Samsoni amesema kipimo cha Zitto
kilishafanyika muda mrefu na ukweli ulishapatika mahakamani alikokuwa
amekimbilia kuweka kinga.
Amesema kuendelea kumsikiliza na
kumwamini mtu anayeonekana wazi kuwa ni msaliti ni sawa na kutwanga pilipili huku
mshahara wake ukiwa ni kukohoa.
“Sioni haja ya kupoteza muda kumsikiliza
msaliti na mroho wa madaraka. Baada ya kuona hapati uenyekiti katika Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akakisaliti chama na hatimaye amepata
alichokuwa anakitaka sasa ameanza kutupumbaza ili aonekane yeye ni kiongozi
makini! Muongo mkubwa kabisa. Cha msingi watanzania tunatakiwa na msimamo
tusiyumbishwe na wanasiasa kama hawa” amesema.
No comments:
Post a Comment