UPATIKANAJI wa damu katika hospitali ya
rufaa ya Iringa pamoja na hospitali za wilaya ni tete kutokana na benki ya damu
kuishiwa damu.
Haya yamezungumzwa na mteknolojia wa
maabara Mkoa wa Iringa Mlike Mwalongo alipotakuwa akihojiwa na waandishi wa
habari ofisini kwake leo juu ya upatikanaji wa damu.
Mwalongo amesema hali ya upatikanaji wa
damu ni tete na kwamba hospitali ya rufaa Iringa pekee inahitaji wastaniwa wa unit 210 kwa mwezi ambapo ni sawa na lita 105
kwa mwezi.
Amesema uhaba wa damu unatokana na
kukosa vitenganishi (vitendea kazi) ambavyo vingewasaidia wataalam wa damu
kufika maeno mbalimbali kwa ajili ya kuwaomba wananchi kuchangia.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni hali ya
uchumi ambapo awali walikuwa wakitegemea wafadhili katika ukusanyaji wa damu
kwa wanaochangia lakini kwa wakati huu wamekosa ufadhili na kusababisha damu
kutopatikana kiurahisi.
“Hali ya upatikanaji wa damu kwa wakati
huu ni tete. Damu haitolewi sehemu moja ila watu wanatembea sehemu mbalimbali
kwa ajili ya kwenda kuomba na kutoa damu kwa watu mbalimbali wanaoguswa na
kuchangia.
“Pia tuna uhaba wa dawa za kupimia damu.
Kwa kuwa upatikanaji wa damu ni tete, tunatumia mbadala kupata damu ili
kumuokoa mgonjwa kwa kuwaomba ndugu wa mgonjwa achangie mgonjwa wake vinginevyo
hatuna jinsi” amesema Mwalongo.
Anabainisha kuwa tatizo la damu
linaloikumba hospitali ya rufaa Iringa ni tatizo la kanda nzima ya nyanda za
juu kusini inayojumuisha mikoa sita ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Katavi na
Rukwa.
Kwa mujibu wa Mwalongo hospitali ya
rufaa Iringa hutumia unit 6 hadi 7 kwa siku ambapo ni sawa na kutumia lita 3.5
kwa siku.