UCHAGUZI wa serikali za Mitaa katika Mtaa wa Ngome Kata ya Kihesa Manispaa ya Iringa umeanza kwa dosari licha ya kulazimika kuanza saa 6:04 mchana kutokana na kucheleweshwa vifaa vya kupigia kura.
Licha ya vifaa vya kupigia kura kuchelewa, bado ilitokea dosari katika karatasi za kupigia kura kwa kile kilochoonekana kwa baadhi ya majina ya waliogombea ujumbe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoonekana kwenye karatasi za kupigia kura na badala yake yakaingizwa majina ya watu wengine ambao hawakujaza fomu za kugombea.
Sambamba na hilo kwa upande wa wagombea kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa na kosa la waliogomea viti maalum kuingizwa jina la mwanaume aliyegombea ujumbe huku mwanamke aliyegombea viti maalumu uingizwa kwenye karatasi la wagombea wa ujumbe.
Sababu hizi zimemlazimu wakala wa Chadema kutokubaliana na utaratibu huo na kutaka utolewe ufafanuzi zaidi kabla ya kuanza zoezi la upigaji kura na kumlazimu msimamizi wa uchaguzi wa kituo hicho kumpigia simu ofisa mtendaji wa Kata ili aweze kutolea ufafanuazi jambo ambalo pia lilimlazimu ofisa mtendaji kurudisha karatasi kwa mkurugenzi ili zifanyiwe marekebisho.
Baada ya maelezo ya ofisa mtendaji wa Kata ya Kihesa Wilbert Chahe kuwa kuna makosa katika karatasi hizo, wananchi walipandisha hasira na kumzingira ofisa huyo jambo lililowawalazimu vijana wa Chadema kumnusuru ili aweze kurudisha karatasi zikarekebishwe.