KLERUU

KLERUU
KLERUU

Ibada

Ibada

Monday, February 23, 2015

WANASIASA NA WAFANYABIASHARA WAHUSISHWA NA MAUAJI YA ALBINO NCHINI TANZANIA


TATIZO la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Albino linalozidi kushika kasi nchini Tanzania linaelezwa kuwa linatokana na watu wenye uchu wa madaraka na mali ambao wamekosa maadili na hofu ya Mungu huku wanasiasa wakihusishwa na jambo hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mtandao huu, wananchi wanaoneshwa kusikitishwa na vitendo hivyo huku wakiitupia lawama serikali kuwa inaonesha uzembe wa makusudi kulichukulia uzito suala hilo.

Sisto Khani mkazi wa Iringa mjini ameuambia mtandao huu kuwa, serikali imeonesha udhaifu katika suala hili kutokana na kutowachukulia hatua kali watuhumiwa wanaokamatwa kwa vitendo hivyo na kwamba kama serikali itaendelea kuonesha udhaifu wa namna hiyo, vitendo hivyo haviwezi kuisha.
Hata hivyo Sisto alisema pamoja na serikali kuonesha udhaifu katika suala hilo, ushirikina ndio chanzo kikubwa cha vitendo hivyo kutokana na watu kuamini kuwa kwa kutumia viungo vya watu hao unaweza kupata utajiri au kutimiza matakwa yao.

“Ushirikina na chanzo cha mauaji ya albino kwa sababu kuna watu wanatumia njia hiyo eti wanataka vyeo, utajiri, mali na uongozi” amesema.

Monday, February 16, 2015

Kesi ya mauaji ya Mwangosi yazidi kuunguruma katika Mahakama Kuu Iringa

KESI ya mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten Daud Mwangosi inayomkabili Pasificus Cleophace Simon imeendelea kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu kanda ya Iringa ambapo mashahidi wawili upande wa Jamhuri waliweza kutoa ushahidi wakiongozwa na wawendesha mashtaka wa serikali Sunday na Ladslaus Komanya.

Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Paul Kihwelo shahidi namba tatu ambaye ni hakimu katika mahakama ya Mwanzo Dodoma mjini Flora Mhelela ameieleza mahakama kuwa Pasificus alifika ofisini kwake wakati alipokuwa hakimu katika mahakama ya mwanzo ya Bomani iliyopo Iringa mjini kwa ajili ya maungamo juu ya kesi inayomkabili.

Ameiambia mahakama kuwa mnamo Septemba 05, 2012 mtuhumiwa kwa kuongozwa na askari ambaye hakumkumbuka jina, alifika ofisini kwake kwa ajili ya maungamo juu ya kesi inayomkabili ambapo ulikuwa ni muda wa saa 07:24 mchana.

Amesema baada ya kupata taratibu zinazotakiwa kufuatwa wakati wa utoaji maelezo mtuhumiwa alikiri kuwa amehiari mwenyewe kutoa maelezo ambapo baada ya kukaguliwa katika mwili wake alikutwa na kidonda kibichi kidoleni pamoja na majeraha makavu.

“Mtuhumiwa aliniambia kwamba mnamo Septemba 2, 2012 ilitokea kazi ambayo alipangiwa kwenda Nyololo ambako kulikuwa na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walikwenda kufanya mkutano.

“Aliendelea kusema kuwa kama ilivyo kawaida kwa ajili ya ulinzi na usalama, kwamba hawakutakiwa kufanya mkutano huo kwa kuwa haukuwa rasmi. Mkutano ulikuwa unazuiliwa kwa sababu kulikuwa na tukio la sensa” ameeleza shahidi namba tatu.

Wednesday, February 4, 2015

VIJANA WAONYWA KUTOKUJIINGIZA KATIKA UFISADI



Jaji Mstaafu Raymond Mwaikasu

VIJANA Wakristo Wakatoliki wametakiwa kutokujiingiza katika vitendo vya ufisadi na badala yake wametakiwa kutumia uhuru waliopewa na Mungu ipasavyo bila kuwakwaza wengine na kwamba viongozi wanaoshindwa kutekeleza majukumu katika haki ni wasaliti wasiowatakia mema wengine.

Haya yamezungumzwa na Jaji Mstaafu Raymond Mwaikasu alipokuwa akiwahutubia vijana wakati wa sherehe za mzimamizi wao Mt. Yohane Bosco zilizofanyika katika ukumbi wa Don Bosco Parokia ya Mkwawa Jimbo lringa.

Jaji Mwaikasu amesema ufisadi umekuwa ni tatizo kubwa katika serikali ya Tanzania na kwamba unasababishwa na watu wasiyo na huruma, wabinafsi, wasiomuogopa Mungu kuwa waroho kupindukia.